Luke 24:1-12

Kufufuka Kwa Yesu

(Mathayo 28:1-10; Marko 16:1-8; Yohana 20:1-10)

1 aMnamo siku ya kwanza ya juma, alfajiri na mapema, wale wanawake walichukua yale manukato waliyokuwa wameyaandaa, wakaenda kaburini. 2 bWakakuta lile jiwe limevingirishwa kutoka kwenye kaburi, 3 clakini walipoingia ndani, hawakuuona mwili wa Bwana Yesu. 4 dWalipokuwa wanashangaa juu ya jambo hili, ghafula watu wawili waliokuwa wamevaa mavazi yanayongʼaa kama umeme wakasimama karibu nao. 5Wale wanawake, wakiwa na hofu, wakainamisha nyuso zao mpaka chini. Lakini wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai miongoni mwa wafu? 6 eHayuko hapa; amefufuka! Kumbukeni alivyowaambia alipokuwa bado yuko pamoja nanyi huko Galilaya kwamba: 7 f‘Ilikuwa lazima Mwana wa Adamu atiwe mikononi mwa watu wenye dhambi na waovu ili asulubiwe, na siku ya tatu afufuke.’ ” 8 gNdipo wakayakumbuka maneno ya Yesu.

9 hWaliporudi kutoka huko kaburini, wakawaeleza wale wanafunzi kumi na mmoja pamoja na wengine wote mambo haya yote. 10 iBasi Maria Magdalene, Yoana, na Maria mama yake Yakobo, pamoja na wanawake wengine waliofuatana nao ndio waliwaelezea mitume habari hizi. 11 jLakini hawakuwasadiki hao wanawake, kwa sababu maneno yao yalionekana kama upuzi. 12 kHata hivyo, Petro akainuka na kukimbia kwenda kule kaburini. Alipoinama kuchungulia, akaona vile vitambaa vya kitani, ila hakuona kitu kingine. Naye akaenda zake akijiuliza nini kilichotokea.

Copyright information for SwhNEN